October 28, 2020

ZLATKO KUISUKA UPYAA, SAFU YA USHAMBULIAJI YANGA

Msomaji wa Yanganews Bkog:Kocha mkuu wa Yanga, Zlatko Krmpotic, amesema sasa amewaandalia programu mpya washambuliaji wake kutokana na kutoridhishwa na idadi ya mabao wanapata katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Safu ya ushambuliaji wa Yanga inaongozwa na Michael Sarpong, Sogne Yocouba, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke, Tuisila Kisinda, Haruna Niyonzima, Carlos Carlinhos na Farid Mussa.

Zlatko alisema timu yake imeanza kucheza vizuri na inamiliki mpira, lakini bado haijakaa vema kwenye idara ya kupachika mabao licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

Kocha huyo alisema mabao mawili ambayo wamefunga katika mechi mbili walizocheza hayatoshi na yanaifanya safu yake ya ushambuliaji kutokuwa na makali.

‚ÄúTumefunga mabao mawili tu, sijaridhika na hali hii, inaonyesha dhahiri wachezaji wangu hasa wanaocheza kwenye robo ya mwisho ya uwanja wanakosa ubunifu wa kutengeneza nafasi, nahitaji wabadilike zaidi,” alisema Zlatko.

Aliongeza katika mechi dhidi ya Mbeya City walifanya mashambulizi mfululizo katika dakika 75, lakini hawakutengeneza nafasi za wazi za kufunga kama inavyotakiwa, hivyo wanahitaji kupewa mbinu zaidi za umaliziaji.

“Nimeona mabadiliko kidogo ila nalazimika tulifanyie kazi haraka kabla hatujaanza michezo yetu ya ugenini, ikiwamo mechi ijayo dhidi ya Kagera Sugar, tumejipanga kwenda kupambana kutafuta alama muhimu pamoja na kupata idadi nzuri ya mabao zaidi ya tulivyofanya kwenye mechi mbili zilizopita,” alisema Zlatko.

Aliutaja mchezo wa kirafiki waliocheza juzi usiku dhidi ya Mlandege ya Zanzibar umemsaidia kuona wachezaji wanavyopokea mafunzo mapya na namna kila mmoja alivyotekeleza majukumu yake na hatimaye kupata ushindi wa mabao 2-0, shukrani kwa Waziri Junior na Mukoko Tonomne waliofunga magoli.

Kikosi cha Yanga tayari kimeshawasili Bukoba tayari kuendelea kujinoa kuelekea mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, utakaochezwa kesho mjini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *