October 23, 2020

CARLINHOS KUENDELEZWA KUPEWA DAKIKA CHACHE YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Licha ya kiungo Carlos Carlinhos, kuchangia ushindi ndani ya dakika 29 alizoichezea Yanga dhidi ya Mbeya City Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, huo ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu tangu ajiunge na klabu hiyo msimu huu, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zlatko Krmpotic amesema ataendelea kumpa dakika chache hadi hapo atakapokuwa fiti.

Katika mchezo huo ambao Yanga ilishinda bao 1-0, Carlinhos aliingia akitokea benchi dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambapo mbali na mashuti yake mawili kushindwa kujaa nyavuni, kona yake ya dakika ya 86 kutoka wingi wa kushoto, iliunganishwa kimyani kwa kichwa na beki wa kati, Mghana Lamine Moro.

Kiwango hicho kimewafanya mashabiki kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kupaza sauti zao wakimtaka Zlatko kuanza kumwanzisha katika kikosi cha kwanza ili kuisaidia timu kupata ushindi.

Lakini Zlatko amesema wachezaji Carlinhos na mshambuliaji Yacouba Sogne, na baadhi yao ataendelea kuwapa dakika chache za katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara hadi hapo watakapokuwa fiti kama anavyohitaji.

Akizungumza na chanzo chetu hapo jana, Zlatko alisema nyota hao walionyesha mabadiliko makubwa na kucheza vizuri, lakini ataendelea kuwapa dakika chache iwe za mwanzo au mwisho za kucheza hadi watakapokuwa fiti.

Alisema kutocheza kwa miezi minne hadi mitano katika nchi walizotoka kutokana na janga la corona lililoikumba dunia, analazimika kuwapa dakika chache za kucheza ili miili yao iwe tayari kuhimili kucheza kwa dakika nyingi.

“Miezi minne hadi mitano kwa mchezaji bila kucheza ni mingi sana, Carlinhos na Yocouba ni wachezaji wazuri na wana uwezo mkubwa wa kusaidia timu kupata matokeo, lakini bado hawajawa fiti zaidi ili kunishawishi kuwapa muda mrefu wa kucheza,” alisema Zlakto ambaye ni raia wa Serbia.

Alisema mashabiki wanatakiwa kuvumilia pamoja na kuwaamini wachezaji wao kwa sababu anaendelea kusuka kikosi cha timu hiyo kuweza kupata matokeo mazuri katika mechi zake.

Kocha huyo alisema ataendelea kuwapa nafasi ya kucheza kila mchezaji kwa ajili ya kuwaweka fiti zaidi ya walivyocheza katika mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City.

“Kuna wachezaji ambao wameonyesha muunganiko mzuri kwa sababu walianza kufanya mazoezi mapema, waliochelewa naendelea kuwapa dakika chache za kucheza,” alisema Zlatko ambaye amerithi mikoba ya Luc Eymael aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu uliomalizika.

Alisema maandalizi yao dhidi ya Kagera Sugar yanaendelea vizuri, na lengo lao ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Jumamosi.

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam leo kuelekea Kagera tayari kwa mchezo huo wa raundi ya tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *