October 28, 2020

YANGA KUKINUKISHA LEO MECHI YA LIGI KUU DHIDI MBEYA CITY

Msomaji wa Yanganews Blog:Yanga juzi Ijumaa ilizindua jezi zao mpya za msimu huu Jijini Dar es Salaam na kwa mara ya kwanza leo zitaonekana Uwanja wa Taifa katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City.

Yanga ambao wameonekana kuhamasika zaidi kila kona ya nchi kununua jezi hizo, leo watakuwa na mwonekano wa kipekee huku Hersi Said mmoja wa vigogo wa kamati ya utendaji akitamba uzi huo umeongeza msisimko miongoni mwa mashabiki na wachezaji na wanategemea ushindi mzuri.

Rekodi mbalimbali za mechi za awali za Ligi Kuu baina ya Yanga na Mbeya City Dar es Salaam zinaibeba Yanga ingawa msimu huu huenda kukawa na mabadiliko makubwa kutokana na usajili mkubwa uliofanywa na klabu zote mbili.

Mpaka jana jioni mechi hiyo ilikuwa imepangwa kuchezwa leo saa 1:00 usiku Uwanja wa Mkapa ingawa kulikuwa na sintofahamu kutokana na mashindano ya Taifa ya Riadha yaliyokuwa yakiendelea hapo.

Hata hivyo, sare ya Yanga na Prisons kwenye mechi ya awali huenda ikaongeza ugumu kwa Mbeya City katika mchezo wa leo kwani Yanga wamepania kujisafisha mbele ya mashabiki wao.

Mshamabuliaji Michael Sarpong ambaye alifunga bao lake la kwanza tangu atue ndani ya kikosi hicho wiki iliyopita dhidi ya Prisons, ataingoza Yanga leo kusaka ushindi wa kwanza msimu huu.

Pia kocha Zlatko Krmpotic anaweza kumuanzisha Mulangola, Carlos Fernandes ‘Carlinhos’katika mchezo wa leo baada ya ule uliopita dhidi ya Prisons kumweka benchi huku akijitetea bado hakuwa fiti kucheza mchezo ule.

Mbeya City ambayo mchezo wa kwanza wa ligi ilikubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa KMC, inaponzwa na ugeni wa wachezaji wengi katika kikosi hicho hivyo kushindwa kucheza kitimu kama ilivyo pia kwa Yanga ingawa wao wana faida ya uzoefu.

Rekodi zinaibeba Yanga dhidi ya Mbeya City katika mchezo huo kwani imekuwa ikipata matokeo mazuri kila inapoikabili timu hiyo jijini Dar es Salaam iwe Uwanja wa Mkapa au Uhuru.

Tangu Mbeya City ipande daraja kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2013, imekutana na Yanga mara saba jijini Dar es Salaam huku Yanga imeshinda mara sita na kupata sare moja.

Yanga imeifunga Mbeya City mabao 16 wakati wakipinznai wao wakitikisa nyavu zao mara tatu tu.

Kipigo kikubwa ambacho Yanga imewahi kuipa Mbeya City jijini Dar es Salaam ni cha Novemba 19, 2017 ilipoitandika mabao 5-0.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema wamajindaa vizuri kuhakikisha wanachukua pointi zote tatu hivyo dakika 90 zitaamua na watacheza soka safi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Zlatko Krmpotic amekiri kwamba kikosi chake kimeanza kuiva hususani mastaa wa kigeni Tuisila Kisinda, Mkoko Tonombe na Michael Sarpong hivyo mashabiki wategemee soka la ushindani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *