October 20, 2020

KOCHA MKUU YANGA ASHINDWA KUJIZUIA, ASIFIA UWEZO WA TUISILA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Kocha wa Yanga, Mserbia Zlatko Krmpotic kuna kitu amekiona kwa wachezaji watatu akijiandaa kuivaa Mbeya City Jumapili usiku.

Zlatko alisema mapambano kwa wachezaji wote wa Yanga ni ya hali ya juu mazoezini na kambini ili kumshawishi lakini, Tuisila Kisinda, Yacouba Sogne na Mukoko Tonombe ni mafundi na mpaka sasa wako vizuri.

“Sina muda mrefu ndani ya timu lakini nikianza katika mechi ya kwanza ambayo tulicheza na Tanzania Prison mtu kama, Tuisila, Sogne na Mukoko walitimiza majukumu yao ipasavyo licha ya kuingia kipindi cha pili,”alisema Kocha huyo ambaye baada ya wikiendi hii atakwenda Kagera kisha Morogoro kwa Mtibwa kabla ya kurudi Dar kuikaribisha Coastal Union.

“Wachezaji hao hawakuishia hapo kwani hata katika mazoezi yetu ya kila siku kila mmoja amekuwa akifanya vizuri katika majukumu ya nafasi yake jambo ambalo nimeona vitu kwao,”alisema.

“Umahiri ambao wameonesha wachezaji hawa mpaka sasa unaweza kunisukuma kuwaanzisha katika mechi inayofuata ili kuona tunapata matokeo mazuri tofauti na yale tuliyoyapata awali.

“Kikubwa ambacho naangalia wakati huu ni kutoa nafasi kwa kila mchezaji ambaye anafanya vizuri katika mazoezi na hata mechi husika ili kuona tunabadilika na kupata pointi tatu bila kujali tumefunga mabao mangapi.

“Kazi nyingine ambayo ipo ni kuhakikisha kila mchezaji anabadilika na kufanya kazi yake kama ipasavyo tena katika kiwango cha juu ili kupata nafasi ya kucheza,” alisema Zlatko.

“Nimeona kuna baadhi ya wachezaji wapo tayari kwa mashindano lakini kuna wengine bado wapo katika viwango vya kawaida wanatakiwa kubadilika katika hilo kwani Yanga ni timu ambayo inahitaji matokeo zaidi kuliko jambo lolote.”

Katika hatua nyingine Zlatko alisema mabadiliko katika timu huwa hayatokei mara moja au haraka ila anahitaji muda kuijenga timu itakayokuwa katika ushindani zaidi.

“Muda huu kuna baadhi ya wachezaji kama Tuisila, Mukoko na Sogne wameonesha mwanga na katika siku zijazo naimani idadi hii itaongezeka kutokana na wachezaji wangu wengi kuwa na vipaji.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *