October 23, 2020

MAMBO YANAZIDI KUNOGA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Yanga juzi jioni iliwapa furaha mashabiki wake katika tamasha la kilele cha Wiki ya Mwananchi baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Aigle Noir katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Chanzo chetu imeangazia namna kikosi cha Yanga kilivyocheza mechi yao hiyo na kuwafanya mashabiki wao wasahau shida zote walizopitia kwa miaka mitatu iliyopita.

MUUNGANIKO

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi kitu cha kwanza ambacho alikisema ameanza nacho ni kutafuta muunganiko wa wachezaji katika kikosi chake.

Alikubali kwamba usajili uliofanywa na mabosi wa GSM ni kati ya usajili bora baada ya kushusha wachezaji wazuri ambao pia wanajua mazingira ya Ligi za Afrika,

Hilo limejionyesha katika mchezo wao dhidi ya Aigle baada ya timu hiyo kuwa na muunganiko wa kutosha kiasi ambacho kwa haraka haraka ungeweza kusema timu hiyo imekaa mwezi kwa pamoja.

UTULIVU

Kikosi cha Yanga kimezidisha utulivu na hii inawezekana imechangiwa na kuongezeka wachezaji ambao wana uzoefu wa kutosha. Hili limejionyesha kwamba licha ya wachezaji wageni kuingia hawajaonekana kama vile wapya bali wamecheza kwa utulivu ambao wakikaa kwa pamoja wiki kadhaa watacheza kwa kiwango cha juu zaidi.

Upande wa mabeki ya kati Bakari Mwamnyeto na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wote ni wapya kwa msimu huu, lakini walikuwa wanacheza kama vile wamekaa kwa pamoja muda mrefu katika kikosi hicho.

Mazoezini kocha Mwambusi alikuwa anampanga Mwamnyeto na Lamine Moro, lakini baada ya Moro kuumia ilimlazimu kumpa nafasi Ninja na hakumuangusha hata kidogo.

PACHA YA MUKOKO, FEISAL

Makocha Mwinyi Zahera na Luc Eymael walikuwa wanapenda kumtumia kiungo Feisal Salum kama kiungo mkabaji na kuwanyima mashabiki wa Yanga raha ya kuona burudani kutoka kwa mchezaji huyo.

Lakini Mwambusi alimpa Fei nafasi ya kucheza kwa kujiachia akisogea mbele huku kwenye upande wa ukabaji akimuachia Tonombe Mukoko.

Mukoko aliyesajiliwa kutokea AS Vita ya DR Congo, ni kiungo ambaye anatumia akili nyingi kwenye ukabaji wake, hatumii nguvu pekee bali anachanganya vyote kwa pamoja kisha anafanya kazi yake vizuri.

Kiungo huyu ana faida mbili anapokuwa uwanjani, kwanza anajua namna ya kuituliza timu anapokuwa na mpira na kuangalia wapi ambapo anaweza kupeleka mpira, pili ni kiungo ambaye anaweza kupiga pasi za mwisho.Katika mchezo wa juzi, Mukoko alimpa kazi nyepesi kiungo Feisal Salum kwani yeye alikuwa anakaba. Jambo hilo lilizaa matunda. Fei alipoga bonge la asisti kwa Tuisila Kisinda.

KUSHOTO, KULIA KOTE SAFI

Yanga ya sasa imepata mabeki wa kushoto na kulia wote wazuri kutokana na usajili waliofanya wa kuwashusha, Yassin Mustapha (Polisi Tanzania) na Kibwana Shomari (Mtibwa Sugar).

Ubora wa wachezaji hawa uliwafanya wachezaji wa Aigle Noir kupata tabu.

Wachezaji hawa walionyesha kiwango kizuri katika kupiga mipira ya krosi kitu ambacho ndio kinahitajika katika kikosi hicho.

Msimu uliopita kwenye timu hiyo, kushoto ilikuwa inamtumia Jaffari Mohamed ambaye awali alikuwa anacheza kama kiungo lakini kocha Mwinyi Zahera alimbadili kabisa nafasi.

Kwa upande wa kulia ikitokea Juma Abdul ameumia, Paul Godfrey ‘Boxer’ alikuwa anakosa nafasi ya kucheza badala yake alikuwa anacheza Deus Kaseke lakini msimu huu inaweza kuwa tofauti kutokana na ‘Boxer’ na yeye kuanza kuwa katika fomu.

KISINDA NA SARPONG

Winga Tuisila Kisinda amewakuna mashabiki wa Yanga kwa kiwango chake juzi.

Mchezaji huyu ni mwepesi mno katika kupeleka mashambulizi, huku akitumia kwa ubora mguu wake wa kushoto.

Kisinda pia ni mchezaji ambaye anajua kucheza kwa nafasi kwani hata goli lake alilofunga katika mchezo dhidi ya Aigle Noir, alionyesha njia kwa kiungo Feisal Salum na kiungo huyo alimpigia pasi mpenyezo ambayo alikutana nayo na kutupia wavuni.

Mshambuliaji Michael Sarpong, ni mchezaji ambaye anajua namna ya kuutumia mwili wake, anaweza kupambana na mabeki kuhakikisha kwamba anawapunguza spidi katika ukabaji wake.

Sarpong anaonekana ni mchezaji ambaye analijua goli. Bao la kichwa alilofunga akitumia krosi ya Ditram Nchimbi ni ishara kwamba kuna mengi yanakuja.

JUNIOR, CARLINHOS

Mshambuliaji Wazir Junior ni mchezaji anayejua kufunga. Lakini katika mchezo huu alikuwa na papara akionyesha kupania sana na matokeo yake kuwanyima wenzake nafasi za kufunga kirahisi akitaka afunge yeye.

Kiungo Carlos Fernandez ‘Carlinhos’ alicheza dakika chache lakini shuti lake kali linaashiria hatanii uwanjani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *