October 28, 2020

ALICHOSEMA KOCHA MPYA YANGA BAADA YA MAZOEZI HAPO JANA

Msomaji wa Yanganews Blog:Kocha mpya wa Yanga, Zlatko Krmpotic alikiongoza kikosi cha Yanga katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria kilichoko jijini Dar es Salaam akiwa na wachezaji wake wote waliosajiliwa akiwamo mshambuliaji mpya kutoka Burkinafaso, Yacouba Sogne, ambaye aliwasili nchini juzi.

Kocha huyo alisema wachezaji wake wamefanya mazoezi vema, lakini anasikitika kukosa muda wa kucheza mechi ya kirafiki ili kuwaimarisha kabla ya kuanza msimu mpya.

“Ingekuwa vema kama tungepata mchezo wa kirafiki, lakini muda ni mfupi kabla ya kuanza kwa ligi, tunaendelea na maandalizi na naamini mambo yataenda katika mstari tunaoutaka,” alisema Zlatko.

Aliongeza kama angepata muda wa wiki mbili au tatu, angepata muda wa kufanya majaribio ambayo yangewaimarisha wachezaji wake na kupata kikosi imara zaidi kitakachokuwa tayari kupambana.

“Kuna programu ya mazoezi nimeiandaa, tutaitumia kwa kipindi hiki kilichobakia ili kuweka muunganiko mzuri kwa wachezaji,” Zlatko alisema.

Meneja , Hafidh Saleh, alisema anaamini kikosi kitaanza vema msimu mpya baada ya kila mchezaji kuwa na kiu ya mafanikio.

“Tuko tayari kwa msimu, ingawa Kocha Zlatko aligusia kupata mchezo wa kirafiki baada ya ule wa Jumapili dhidi ya Eagle Noir, lakini muda umekuwa mfupi,” alisema Saleh.

Yanga itaanza kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwakaribisha ‘Maafande’ wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini.

1 thought on “ALICHOSEMA KOCHA MPYA YANGA BAADA YA MAZOEZI HAPO JANA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *