October 25, 2020

ALICHOSEMA MWENYEKITI YANGA KUELEKEA WIKI YA MWANANCHI

Msomaji wa Yanganews Blog:Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla ametamka wataujaza uwanja mapema bila wasiwasi wowote.

Yanga leo inahitimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi ambayo msimu huu ilizinduliwa mkoani Dodoma kwa wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo za kijamii kama kutembelea wagonjwa, yatima na walemavu na kutoa misaada mbalimbali.

Msolla anasema wanakwenda kusimamisha nchi pale kwa Mkapa hawatarajii kuwe na gepu, mashabiki waende kuujaza uwanja na kuona vifaa ambavyo uongozi kwa kushirikiana na mdhamini wao ulijifungia na kuvifanyia kazi kabla ya kuvileta nchini kuitumikia timu ya Wananchi.

“Ile hamasa wakati wa kuwapokea wachezaji iwe maradufu tuujaze uwanja, kusiwe na gepu,iwe salamu kuwa Yanga ni timu ya Wananchi, lakini hamasa hiyo iendelee hadi kwenye ligi,” anasema na kusisitiza anaamini hilo litawezekana kutokana na hali halisi anayoiona kwenye matawi nchi nzima na mitaani.

Anasema lengo ni kuhakikisha leo mchezaji akigeuka na kuona viti vimejaa ajue kwenye ni timu ya wananchi

“Msimu uliokwisha hatukuwa vizuri,tulifanya kosa kwenye usajili, klabu kuwa na wachezaji 10 wa kigeni halafu wazuri ni wawili, ile iliwanyong’onyesha wapenzi na wanachama, licha ya kwamba tulipambana tukamaliza ligi kwenye nafasi ya pili.

“Klabu kwenda kuvunja mkataba wa mchezaji wa kimataifa na kumsajili si jambo dogo, Yanga sasa ni kama klabu za Italia,” anasema na kuongeza wanategemea soka la aina yake msimu huu.

Uongozi wa Dk Msolla umetimiza miezi 16 na wiki kadhaa tangu ulipochanguliwa Mei mwaka jana, kiongozi huyo anasema walipoingia madarakani, walikuta kamati ya mpito ya hamasa imepanga shughuli ya futari na ile ya kubwa kuliko ambazo zilifanyika kwa mafanikio.

“Baada ya kilele cha Kubwa kuliko tulikaa na kukubaliana kuwa tuongeze Wiki ya Mwananchi ambayo ki ukweli licha ya kwamba msimu huu tunaifanya kwa mara ya pili, lakini imekuwa na tija mno kwa klabu,” anasema.

Mkakati wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu Msolla anasema baada ya kilele cha Wiki ya Mwananchi leo, kutakuwa na andiko la kwanza la muundo mpya wa klabu.

KIUFUNDI

Kocha Juma Mwambusi akisaidiana na kocha Said Maulid ‘SMG’ ndio wataiongoza Yanga leo baada ya kuwa mazoezini na mechi za kirafiki ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya na mechi hii ya kilele cha wiki ya Wananchi amewaondoa shaka mashabiki wa Yanga kwa usajili ambao umefanywa na mabosi wa klabu hiyo katika kuijenga timu.

Katika mazoezi ya juzi Ijumaa kabla ya jana jioni katika uwanja wa Mkapa, Mwambusi aliwapanga katika kikosi cha kwanza, Faroukh Shikhalo, Kibwana Shomari, Yasin Mustafa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Deus Kaseke, Feisal Salum, Michael Sarpong, Waziri Junior na Deus Kaseke.

Kikosi hiki kilikuwa na kombinesheni nzuri ya kucheza kwa maelewano, huku Ninja ambaye amechukua nafasi ya Lamine Moro aliyeumia, kuweza kumudu vizuri nafasi hiyo hasa kwenye kucheza mipira kwa kulala.

VIINGILIO

VVIP 200,000

VIP A 30,000

VIP B 20,000

Mzunguko 5000

VITUO VINAVYOUZWA TIKETI

Makao makuu ya klabu, Karume TFF, Buguruni Sheli, Dar Live, Mbagala, Ubungo Sheli, Mwenge Puma, Kigamboni Feri, Mlimani City, Uwanja wa Uhuru, Kariakoo Big Bon Sheli, Gongo la Mboto sheli, Mbezi Mwisho, Mwembe Yanga na GSM Mall.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *