October 20, 2020

HUYU HAPA BEKI AAHIDI KULIPA FADHILA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Beki wa kati Ladislaus Mbogo aliyesajiliwa Yanga, lakini hakucheza hata mechi moja kutokana na kufanyiwa upasuaji wa uvimbe kwenye shavu? Basi jamaa ameibuka na kutamka kuwa, anataka kulipa fadhila kwa timu hiyo kwani ilimtendea mema.

Iko hivi msimu 2012/13 Yanga ilimsainisha beki huyo akitokea Toto Africans kwa mkataba wa mwaka mmoja, lakini uongozi wa timu hiyo ukaona ni vyema kumfanya upasuaji wa uvimbe mkubwa uliokuwa upande kushoto wa shavu lake.

Mbogo alizaliwa na uvimbe huo uliokuwa unamtesa kutokana na maumivu aliyokuwa anayapata, lakini alipotua Yanga tu waliamua kumpa faraja kwa kumfanyia upasuaji huo.

“Furaha yangu ilirudi baada ya ule upasuaji kwa kweli Yanga nitaikumbuka katika maisha yangu, natamani nije kulipa fadhila kama nitashindwa kucheza basi iko siku nitarudisha shukuani zangu kwa jambo lingine la kihistoria kabisa.

“Unajua baada ya ule upasuaji nilikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu nikiuguza kidonda hivyo, msimu ukaisha bila ya kucheza na baada ya hapo nikaenda Rhino Rangers hivyo, sikucheza hata mechi moja kitu ambacho kinaniumiza sana,” alisema Mbogo

Msimu uliopita beki huyo hakusajiliwa na timu yoyote baada ya kuachana na klabu ya Olympic Stars ya Burundi ambapo, sasa yuko fiti na anapambana kujifua ili kunasa timu kwenye Ligi Kuu Bara.

“Sasa nimerudi nyumbani na natafuta timu ya kucheza kwani, bado kiwango changu kipo sawa hivyo kwa timu inayotaka kuja kufanya mazungumzo na mimi zinaweza kuja na tutafikiana makubaliano,” alisema beki huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *