October 31, 2020

TUISILA, TUNOMBE WATIKISA JIJI

Msomaji wa Yanganews Blog:Nyomi la mashabiki wa Yanga wamegeuka gumzo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambako wamekuja kuwapokea wachezaji wao wawili wapya, Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe.

Nyota hao wawili wanatua mchana wa leo Alhamisi Agosti 20, 2020 wakitokea DR Congo tayari kuungana na kikosi cha Yanga ambacho kimewasajili kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Mashabiki hao wa Yanga walianza kujazana nje ya uwanja huo kuanzia saa saba kasoro na baada ya hapo waliingia kwa wingi uwanjani wakiimba na kukimbia mchakamchaka.

Nyimbo hizo ambazo walikuwa wakiimba, zilikuwa zikiwataja Kisinda na Tonombe waliojiunga na timu yao wakitokea AS Vita ya DR Congo pia wadhamini wa klabu hiyo, kampuni ya GSM ambayo ndio imesimamia usajili wao.

“Nani kaua, Kisinda. Nani kaua GSM. Nani kaua, Tonombe. Wape salam wape Salam,” walisikika mashabiki hao.

Walipofika uwanjani hapo, walijazana karibu na mlango wa kutokea abiria wanaowasili na kuendelea kuimba jambo lililowalazimu maofisa usalama kuwaomba wasogee mbali na mlango huo ili kutowapa usumbufu abiria.

Kutokana na tangazo hilo, mashabiki hao walitii agizo hilo na kusogea nyuma kidogo huku wakiendelea kuimba nyimbo zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *