October 23, 2020

FARID MUSSA AFUNGUKA, SABABU KUJIUNGA NA YANGA, KUPIGA CHINI OFA KIBAO

Msomaji wa Yanganews Blog:Farid Mussa amesaini dili la kuitumikia Yanga ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, akitokea CD Tenerife ya Ligi Daraja la Kwanza Hispania.

Chanzo chetu ilimfuata nyumbani kwake Farid ambaye anaishi Chamazi jijini Dar es Salaam ili kufahamu Mchakato wa kujiunga na Yanga ulikuwaje

MAMBO YALIANZIA HAPA

Baada ya kucheza soka kwa miaka minne nchini Hispania huku akiona giza mbele yake, Farid anasema hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kusuburi mkataba wake umalizike ili aachane na klabu hiyo.

“Baada ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 nilipata ofa nyingi lakini zile klabu zilizokuja kuongea na Tenerife zilikuwa zikihitaji kiwango kikubwa cha fedha na ukizingatia sikuwa na mkataba nao wa miaka mingi hivyo ilishindiakana kuondoka.

“Nilijipa uvumilivu ili kusubiri mkataba wangu umalizike ndio nifanye mazungumzo na hizo timu,” anasema Farid.

CORONA YATIBUA

Farid anasema mkataba wake ulipomalizika ndio wakati ambao timu nyingi uwezo wao wa kiuchumi uliposhuka. “Nilijiona kuwa na gundu kwa sababu klabu nyingi zilikuwa zikipitia wakati mgumu kiuchumi, kutokana na ugonjwa wa covid 19 uliyosababisha hilo, hivyo ilikuwa ni ngumu kuanza mazungumo na hizo klabu.

“Nikaona nirudi nyumbani kwanza ili kuendelea kufuatilia taratibu mipango yangu ya kupata klabu nyingine nje, sikuwa na mawazo kichwani mwangu kuwa nitarudi kucheza soka nyumbani,” anasema.

TENERIFE YANG’ANG’ANA

Wakati ambao Farid anajiandaa kurejea nyumbani, anasema klabu yake ya CD Tenerife ilimwita na kukaa naye chini ili kufanya mazungumzo ya mkataba mpya, kwamba walikuwa tayari kumwongezea hata kiwango cha mshahara ambacho alikuwa anakihitaji.

Kwa wakati wote wa miaka minne ambayo alikuwa akicheza soka la kulipwa Hispania, Farid aliishia kucheza soka akiwa kikosi B cha timu hiyo ambacho kilikuwa kikishiriki Ligi Daraja la Tatu nchini humo maarufu kama ‘Tercera’.

“Niliwapa sharti moja kubwa kama mnataka niendelea kuwa hapa nataka mnihakikishie kucheza kikosi cha kwanza na sio tena kikosi B, hawakuwa na majibu ya kueleweka, wapo ambao walisema nifanye mazoezi na kikosi cha kwanza alafu mechi nicheze kikosi B, nikaona kuwa ni upuuzi,” anasema winga huyo wa zamani wa Azam FC.

KUMBE WALITEGA MASLAHI

Wakati akiwa katika mch-akato wa kurudi nyumbani, Farid aligundua kuwa viongozi wa kikosi B waliku wa wakim-ng’ang’a nia kuendelea kuwa naye kwenye kikosi hicho kutokana na sababu za kimaslahi.

Kwa nini? Anasema ni kwa sababu kama angeisaidia timu ile ya kikosi B kupanda daraja na kwenda madaraja ya juu ni wazi kuwa wangepiga mpunga mrefu kwa kuuza hisa za timu hiyo.

“Haiwezekani timu ya kikosi cha kwanza na B kucheza ligi moja kwa hiyo walikuwa wanataka tuipandishe daraja timu ili wauze hisa kwa timu ambayo ilikuwa ikihitaji ile nafasi,” anasema.

HERSI AMTWANGIA SIMU

Baada ya kurejea nyumbani Tanzania akiwa na mipango yake, Farid anasema alistukia ikiingia simu ya mtu aliyejitambulisha kama Injinia Hersi Said, alimchangamkia kama ilivyo kawaida yake na kumwuliza uwezekano wa kuipata saini yake.

“Niliwaomba wanipe wiki mbili kwa sababu nilikuwa nikifuatilia mambo yangu, nilikuwa nikifuatilia madili yangu ya nje, ilishindikana kupata nafasi kama ambavyo nilikuwa nikitarajia kwasababu kama ambayo nilisema mwanzo klabu nyingi zimeyumba,” anasema.

VIGOGO AZAM WAJITOSA

Haikuishia kwa Yanga, klabu yake ya zamani ya Azam FC nayo ilionekana kutaka huduma yake, Farid anasema alipigiwa simu na mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ na kumuomba arejee nyumbani ili waunganishe nguvu ya pamoja wakimtaka acheze hata msimu mmoja.

“Nilimwomba anipe muda na kumwambia nitawapatia jibu. Wakati huo bado nilikuwa napambana na kusaka timu za nje “anasema Farid ambaye alizaliwa Juni 21, 1996 mkoani Morogoro.

SIMBA WATANGAZA DAU

Wakati ambao mambo yake ameona hayajakaa sawa huku Yanga na Azam zikionyesha nia ya kutaka kumsajili, Farid anasema Simba nao wakaingia kwenye vita ya kuiwania saini yake, hivyo akawa anatafakari mambo ya msingi kabla ya kufanya uamuzi wowote.

“Simba nao walionyesha kutaka kunisajili, nikawa njia panda sasa sijui nifanye uamuzi gani. Niliona ni bora nicheze kwanza nyumbani hata msimu mmoja ili milango ikikaa sawa nichomoke tena,” anasema.

ASHAURIWA ATUE YANGA

Farid hakukurupuka kufanya iamuzi ya kujiunga Yanga, ambako amesaini mkataba wa muda mfupi huku akizipotezea Simba na Azam kwa mujibu wa aliyemshauri anasema ni rahisi kwake kung’ara akiwa na timu ya wananchi kwa sababu ndio kwanza inajengwa.

“Nilikaa na rafiki yangu ambaye nimekuwa nikishauriana naye mambo mengi na kumweleza kila kitu kinachoendelea, tukazichambua ofa ambazo zipo mbele yangu, akaona ni vema nikasaini Yanga kwa sababu ndio kwanza timu inajengwa.

“Pia kuangalia hilo na ukubwa wa Yanga mbele ya Azam nikaona ni bora nijiunge na Yanga kwa sababu hata wakati ambao nachomoka wakisikia natokea Yanga halitakuwa jina geni masikioni mwao kwa sababu ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika.” anasema.

MZUKA WA DABI

Oktoba 18 ndio siku ambayo Yanga watakuwa wenyeji wa Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Farid anasema siku zote amekuwa akipenda michezo mikubwa kwake hilo ni jukwaa la kuonyesha madini yake.

“Mchezaji mkubwa siku zote lazima uonyeshe uwezo kwenye michezo mikubwa. Nitatumia uzoefu wangu na uwezo nilionao kuhakikisha naisaidia timu yangu. Itakuwa ni mara yangu ya kwanza kucheza dabi lakini kuhusu presha nimecheza michezo mingi yenye presha ya namna hiyo,” anasema.

HAKUNA JIPYA

Farid anasema hakuna kipya cha kujifunza kwake kuhusiana na soka la Ligi Kuu Bara licha ya kukaa nje kwa miaka minne.

“Mpira wa Tanzania naujua vizuri kwa sababu niliwahi kucheza nikiwa na Azam, najiandaa kuwa fiti kwa sababu nikiwa Hispania Ligi ilisimama hivyo nimekaa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa, nikiwa fiti tutakimbizana hadi basi,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *