October 23, 2020

MWAMNYETO AAHIDI KAZI KAZI KIKOSINI YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:kikosi cha Yanga jana kiliendelea na mazoezi ya kujiwinda na msimu mpya wa ligi bara huku wachezaji wapya wa kikosi hicho wakishindana kuonesha uwezo kwenye mazoezi hayo.

Mazoezi hayo yalifanyika Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo Mawasiliano Dar, ambapo licha ya mvua ya rasharasha kutaka kutibua mazoezi hayo lakini baadae mambo yalikaa sawa.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo beki mpya wa kikosi hicho, Bakari Mwamnyeto aliyetokea Coastal  Union ya Tanga amesema anajua ugumu wa kupata namba kwenye kikosi hicho lakini amejiandaa kikazi kuhakikisha anapata namba ya kudumu kikosi cha kwanza.

“Najua sasa hivi nipo kwenye timu kubwa yenye changamoto ya namba lakini nitahakikisha najituma zaidi ya nilivyokuwa ili kuwafurahisha mashabiki wa timu yangu”.

“Hii ni timu kubwa hivyo dawa ya kuwa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza inabidi uoneshe uwezo wa hali ya juu na hilo ndilo lengo langu”amesema

Naye kipa wa timu hiyo, Farouk Shikalo raia wa Kenya ambaye msimu uliopita alikuwa na changamoto namba katika kikosi cha kwanza amewasifu makipa anaoshirikiana nao, Ramadhani Kabwili na Metacha Mnata ambao walimpa changamoto na kuahidi kufanya vizuri zaidi msimu ujao.

“Metacha na Kabwili ni makipa wazuri na msimu uliopita walifanyakazi yao vizuri ndiyo maana kukawa na changamoto ya namba lakini msimu nitahakikisha najituma kadili ya uwezo wangu”. Alisema Shikalo

Msemaji wa timu wa Yanga,Hassan Bumbuli akizungumza baada ya mazoezi hayo amesema kikosi hicho kitakuwa na mechi ya kirafiki kwa ajili ya kukiangalia kikosi chao kipya na timu ambayo ataitaja hapo baadae.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *