November 27, 2020

LEO PATACHIMBIKA CCM KIRUMBA

Msomaji wa Yanganews Blog:Baada ya juzi kuifumua Polisi Tanzania kwa bao 1-0, leo Yanga inatarajia kujitupa tena dimbani kuvaana na KMC katika kutafuta ushindi wa sita wa ligi msimu huu kwenye mechi ya saba tangu kuanza kwa msimu mpya wa 2020-21.

Huo utakuwa mchezo wa pili kwa kocha mpya wa Yanga, Cedric Kaze ambaye amefaulu vizuri mtihani wake wa kwanza dhidi ya Polisi Tanzania huku akitazamiwa kuendeleza wimbi hilo la ushindi tena leo na kuzidi kuitengenezea Yanga mazingira mazuri kuelekea kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kaze amesisitiza kuwa bado ana kazi ya kufanya kwa ajili ya kuleta ushindi katika kila mchezo msimu huu lakini anashukuru kwa ari aliyowakuta wachezaji wa kikosi hicho pamoja na moyo wa akujituma waliokuwa nao.

“Bado tunataka kupiga hatua ya maendeleo kila baada ya mechi, si kweli kwamba mbinu mpya au aina mpya ya uchezaji inaweza kuingia haraka kwa kiasi hicho lakini nashukuru hapa mwanzo kumekuwa na maelewano mazuri.

“Ukitazama hata mechi iliyopita dhidi ya Polisi, wachezaji wamekuwa na ule uvumilivu wa kusuka mipango na kutulia na pia kutafuta nafasi za kufunga kama uliona taratibu tunatengeneza nafasi ya eneo la tatu la kufunga na ninaamini tutakaa vizuri sana eneo hilo muda si mrefu.

“Lakini nafikiri hii mechi inayofuata ni mechi nyingine na inahitaji kupambana zaidi kutokana na wapinzani wetu na dhumuni letu ni kupiga hatua kila baada ya mechi na kupata pointi tatu, hilo ndiyo muhimu kwanza kwa sasa,” alisisitiza Kaze.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *