November 27, 2020

KAZE AAHIDI MAMBO MAZURI YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Kocha mpya wa Yanga, Cedric Kaze amewaambia mashabiki kwamba amesikia shangwe zao baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, sasa ameahidi kuwapa furaha zaidi kwani ndiyo kwanza ameanza.

Hiyo ilikuwa ni mechi yake ya kwanza tangu afanye mazoezi ya wiki moja na kesho Jumapili atakuwa Mwanza kuikabili KMC ndani ya CCM Kirumba.

Kaze aliiambia chanzo chetu kwamba: “Ndiyo kwanza tumeanza, mambo mazuri yanakuja.”

Kocha huyo amesisitiza kwamba mkakati wake namba moja ni kupangua mchezo mmoja baada ya mwingine na amewataka wachezaji kila mchezo wacheze kama fainali kwani mchuano ni mkali.

Alisema amefurahia kiwango na aina ya uchezaji walioanza nao wachezaji wake, lakini anahitaji kufanyia kazi zaidi pasi za mwisho, umiliki wa mpira na kuurejesha mpira ukishaporwa na kucheza kwa kasi. “Nataka kuona kila mmoja anapiga pasi na kumiliki mpira kuanzia nyuma mpaka eneo la timu pinzani.”

Alisema: “Hata kama tutakuwa tunacheza na timu ambayo inatukaba katika eneo letu, sitaki kuona mchezaji wangu anabutua mpira, nataka kuona tunapiga pasi kuanzia katika eneo letu mpaka kufika kwao na kama ikitokea kubutua basi iwe mahala kwenye ulazima wa kufanya hivyo.

“Ukiangalia katika mechi tano ambazo zimepita Yanga walizocheza kwenye ligi bila uwepo wangu ni tofauti kabisa na mpira ambao tulicheza na Polisi Tanzania licha ya ubora wao na uwezo wa kukaba tulimiliki mpira na kupiga pasi kuanzia nyuma mpaka kufika kwao na tukafanikiwa kupata bao.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *