November 27, 2020

KAZE AFURAHIA UPAMBANAJI WA WACHEZAJI YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Kocha wa Yanga, Cedric Kaze amesema kupata matokeo mazuri ndani ya siku tano ni kitu kigumu ila amefurahi namna wachezaji wake walivyoonesha tumaini japo kidogo la kushika mfumo wake.

Kaze alipata ushindi wake wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni siku chache tangu ajiunge nao kuchukua mikoba ya aliyefungashiwa virago, Zlatiko Krmpotic.

Akizungumza hapo juzi baada ya mchezo huo alisema kuna baadhi ya vitu vimemfurahisha kama vile wachezaji kuonesha juhudi kwa kufanya kile alichowaelekeza ingawa kuna muda walikuwa wanasahau.

“Vipindi viwili vilikuwa havifanani jinsi nilivyokuwa nataka, cha kwanza hatukufanya vizuri tulikuwa tunapoteza pasi lakini pia, tulipata nafasi kama tatu za kufunga mabao hatukumalizia vizuri na kipindi cha pili tulijitahidi kiasi, ila najua watazoea taratibu,” alisema.

Alisema kilichomfurahisha zaidi ni vile wachezaji wake walivyojitahidi kucheza mpira mwanzo mpaka mwisho na kupata pointi tatu muhimu.

Kaze alisema matarajio yake ilikuwa ni ushindi, alitamani kuona wachezaji wakitembea na mpira na kumiliki kitendo ambacho wamejitahidi, lakini sio kama alivyotaka akisema ni suala la muda tu watazoea taratibu.

Alisema wanachoangalia kwa sasa ni mchezo ulioko mbele yao dhidi ya KMC kujipanga kwenda Mwanza kwa ajili ya kupigania pointi tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *