December 6, 2020

KAZE AWATOA HOFU WANAYANGA, SAFU YA USHAMBULIAJI YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Huku akiweka mkazo katika maeneo matatu muhimu, Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze, ameeleza yalipo mabao ya washambuliaji wake Michael Sarpong na Sogne Yacouba ambao wanaongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Hadi sasa Sarpong amefunga bao moja tu, alilolipata katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Tanzania Prisons wakati Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1, wakati hali ikiwa hivyo pia kwa Yacouba ambaye naye ameziona nyavu mara moja wakishinda 3-0 dhidi ya Coastal Union, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Hali hiyo imekuwa ikizua hofu kwa mashabiki wa klabu hiyo kuhusu ubutu wa makali yao, lakini Kaze amewatetea Sarpong na Yacouba, akieleza kwanza ni wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho huku akiwatoa hofu Wanayanga kwa kueleza kuwa ni washambuliaji wazuri wasubiri wataona moto wao.

“Sikiliza, Sarpong na Yacouba wote ni washambuliaji wazuri na wanalijua goli vizuri, aliyependekeza wasajiliwe ni mimi baada ya kuwafuatilia muda mrefu.

“Kinachowasumbua ni kukosa mbinu pamoja na viungo wa kuwatengenezea pasi za kufunga, hicho ndicho kimesababisha hayo yote kutokea. Naamini nitawabadilisha kila kitu na ubora wao utaonekana,” alisema Kaze.

Na wakati huu Kaze akikiandaa kikosi hicho kuelekea mechi ya keshokutwa, Alhamisi dhidi ya Polisi Tanzania, ameweka msisitizo katika maeneo matatu ambapo ameonekana kugeukia zaidi stamina, kasi na umiliki wa mpira huku akieleza kutarajia kuona mabadiliko hayo kuanzia mchezo huo ujao.

Akizungumza na chanzo chetu hapo jana, Kaze aliyewasili nchini Oktoba 15, alisema pamoja na kwamba muda aliokaa na wachezaji hao ni mchache, lakini anatarajia mabadiliko makubwa kwenye mchezo wa keshokutwa.

“Kama nilivyosema awali, yapo mambo ambayo nitayatilia mkazo kwa ajili ya mabadiliko ya timu, ndio hayo nimeanza nayo, nitaendelea nayo mpaka pale kutakapoonekana mabadiliko,” alisema.

Alisema anafahamu upinzani mkali uliopo baina ya timu yake na mahasimu wao, Simba ambao wanatarajia kuumana nao Novemba 7, mwaka huu, lakini yeye haifundishi timu kwa ajili ya mechi moja.

“Tuna wiki tatu kama sikosei kabla ya mchezo huo, lakini kwangu mimi Yanga siifundishi kwa ajili ya mchezo huo tu, naandaa timu icheze soka zuri la kasi na lenye matokeo chanya kwa michezo yote ya mbele yetu na jambo hilo linawezekana kabisa,” alisema kocha huyo ambaye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania utakuwa wa kwanza kwake kuiongoza Yanga.

Alisema  anafurahishwa na wachezaji wake kwa namna walivyowaelewa kwenye mazoezi anayowapa jambo ambalo linampa faraja ya kufikia malengo yake.

Kaze ataanza kuiongoza Yanga yenye pointi 13 kutokana na kushinda michezo yake minne na kutoka sare mchezo mmoja katika mitano iliyocheza hadi sasa, na baada ya mechi hiyo wataifuata KMC FC katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *