August 13, 2020
Breaking News

PLUIJM AWEKA HADHARANI, YUPO TAYARI KUREJEA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Pluijm ni mmoja wa makocha waliowahi kuiongoza Yanga kwa mafanikio, lakini aliondolewa na baadaye kwenda kufanya kazi Singida United ya Singida na Azam FC ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na chanzo chetu hapo jana, Pluijm, alisema anasikitika kuona Yanga ‘imepotea’ tangu alipoondoka na endapo inataka kushinda mataji isifanye makosa katika kuchagua kocha mwingine atakayekiongoza kikosi cha timu yao.

Pluijm alisema anaifahamu vema timu hiyo pamoja na soka la Tanzania, hivyo kwake hatakuwa na wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yake endapo atarejea nchini kufanya kazi.

“Ni juu yao, uamuzi ni wao, wao ndio wanajua wanataka klabu yao iende wapi, wanatakiwa kuwa makini kama wanataka mataji, hakuna kubahatisha,” alisema Pluijm.

Mholanzi huyo alisema Yanga inatakiwa kuanza mapema maandalizi ya msimu ujao kwa sababu muda uliobakia kuelekea msimu mpya ni mdogo kwa sababu ya matatizo ya corona yaliyotokea hivi karibuni.

“Mpira wa miguu unachezwa hadharani, hauhitaji majaribio au miujiza, ni lazima maandalizi sahihi yafanyike, ukifanya hivyo, utatarajia matokeo mazuri, usipofanya, usitarajie makombe, itakuwa ngumu,” alisema kocha huyo.

Aliweka wazi kwa sasa yuko huru, hana timu na anafanya shughuli zake binafsi kwenye makazi yake nchini Ghana.

“Sina timu, niko huru, nimepata salamu za kutakiwa lakini si rasmi, kama tutazungumza na viongozi na kufikia makubaliano, nitakuwa tayari kuja tena Tanzania, maisha ya mpira ni ya kuzunguka, unaweza kwenda mbali au ukarudi kule ulikotoka, kikubwa ni kuweka alama nzuri kila unapofanya kazi,” Pulijm alisema.

Yanga ilitangaza kuachana na Eymael mapema wiki hii baada ya kocha huyo kutoa kauli za kibaguzi na hivyo klabu hiyo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza itamshtaki kwenye Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa).